20. Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi.
21. Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena.
22. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari.
23. Jua lilikuwa limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari.
24. Ndipo BWANA akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa BWANA.
25. Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile.
26. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.
27. Ibrahimu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA,
28. naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuru.
29. Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu.
30. Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili.
31. Yule mkubwa akamwambia mdogo, Baba yetu ni mzee, wala hakuna mtu mume katika nchi atuingilie kama ilivyo desturi ya dunia yote.
32. Haya, na tumnyweshe baba yetu mvinyo, tukalale naye, ili tumhifadhie baba yetu uzao.