4. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.
5. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema.
6. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate.
7. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa.
8. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala.
9. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani.
10. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake.