Mwa. 17:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.

6. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako.

7. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.

8. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.

9. Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.

10. Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa.

11. Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi.

12. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako.

13. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.

14. Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.

15. Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara.

16. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake.

17. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa?

18. Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.

Mwa. 17