Mwa. 1:4-15 Swahili Union Version (SUV)

4. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza.

5. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja.

6. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.

7. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.

8. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.

9. Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo.

10. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

11. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo.

12. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

13. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.

14. Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka;

15. tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo.

Mwa. 1