Mt. 8:9-21 Swahili Union Version (SUV)

9. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.

10. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli.

11. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

12. bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

13. Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile.

14. Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa.

15. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia.

16. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,

17. ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu,Na kuyachukua magonjwa yetu.

18. Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo.

19. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako.

20. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.

21. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu.

Mt. 8