54. Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?
55. Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate.
56. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
57. Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee.
58. Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho.
59. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua;
60. wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi.
61. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu.
62. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?
63. Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.
64. Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.
65. Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake;