16. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka.
17. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa;
18. kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo.
19. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate.
20. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha.
21. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya;
22. ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa.
23. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.
24. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji.
25. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.
26. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia.
27. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani,
28. akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye.
29. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
30. Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha.
31. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula.
32. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu.