11. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao.
12. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu.
13. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.
14. Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake.
15. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii.
16. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka.
17. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa;
18. kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo.
19. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate.
20. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha.