1. Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.
2. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;
3. makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;
4. kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.
5. Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.
6. Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;
7. akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.
8. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.
9. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.
10. Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
11. Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha.
12. Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao.
13. Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini.
14. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea.