5. Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.
6. Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,
7. Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?
8. Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu?
9. Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?
10. Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),
11. Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.
12. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.
13. Akatoka tena, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha.
14. Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata.