63. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi?
64. Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa.
65. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi.
66. Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu,
67. akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu.
68. Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika.
69. Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao.
70. Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe.
71. Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena.