59. Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.
60. Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?
61. Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?
62. Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.
63. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi?
64. Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa.
65. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi.
66. Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu,
67. akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu.
68. Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika.
69. Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao.
70. Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe.