Mk. 14:42-59 Swahili Union Version (SUV)

42. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.

43. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee.

44. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.

45. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.

46. Wakanyosha mikono yao wakamkamata.

47. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

48. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang’anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi?

49. Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia.

50. Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.

51. Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata;

52. naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi.

53. Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi.

54. Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani.

55. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione.

56. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana.

57. Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema,

58. Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.

59. Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.

Mk. 14