Mk. 14:35-49 Swahili Union Version (SUV)

35. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke.

36. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.

37. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja?

38. Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.

39. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo.

40. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu.

41. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi.

42. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.

43. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee.

44. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.

45. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.

46. Wakanyosha mikono yao wakamkamata.

47. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

48. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang’anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi?

49. Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia.

Mk. 14