Mk. 14:18-32 Swahili Union Version (SUV)

18. Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti.

19. Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi?

20. Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe.

21. Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.

22. Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu.

23. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.

24. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.

25. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.

26. Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.

27. Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa,Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika.

28. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.

29. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi.

30. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.

31. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.

32. Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo.

Mk. 14