Mk. 13:7-23 Swahili Union Version (SUV)

7. Nanyi mtakaposikia habari za vita na uvumi wa vita, msitishwe; hayo hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.

8. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko ya nchi mahali mahali; kutakuwako na njaa; hayo ndiyo mwanzo wa utungu.

9. Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao.

10. Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote.

11. Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu.

12. Na ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, na baba atamsaliti mtoto, na watoto watashambulia wazazi wao, na kuwafisha.

13. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kusaburi hata mwisho, ndiye atakayeokoka.

14. Lakini mlionapo chukizo la uharibifu likisimama pasipolipasa, (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;

15. na mtu aliye juu ya dari asishuke, wala asiingie kuchukua kitu nyumbani mwake;

16. naye aliye shambani asirudi nyuma kulichukua vazi lake.

17. Lakini ole wao wenye mimba, nao wanyonyeshao siku hizo!

18. Ila ombeni yasitokee hayo wakati wa baridi.

19. Kwa maana siku hizo zitakuwa na dhiki, jinsi isivyokuwa tangu mwanzo wa kuumba alipoumba Mungu hata sasa, wala haitakuwa kamwe.

20. Na kama Bwana asingalizikatiza siku hizo, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule aliowateua amezikatiza siku hizo.

21. Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki;

22. kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule.

23. Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele.

Mk. 13