1. Maneno ya Aguri bin Yake; mausia mtu huyu aliyomwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali.
2. Hakika nimekuwa kama mnyama, wala si mtu;Wala sina ufahamu wa mwanadamu;
3. Wala sikujifunza hekima;Wala sina maarifa ya kumjua Mtakatifu.
4. Ni nani aliyepanda mbinguni na kushuka chini?Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake?Ni nani aliyeyafunga maji ndani ya nguo yake?Ni nani aliyefanya imara ncha zote za nchi?Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua?
5. Kila neno la Mungu limehakikishwa;Yeye ni ngao yao wamwaminio.
6. Usiongeze neno katika maneno yake;Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.
7. Mambo haya mawili nimekuomba;Usininyime [matatu] kabla sijafa.
8. Uniondolee ubatili na uongo;Usinipe umaskini wala utajiri;Unilishe chakula kilicho kadiri yangu.
9. Nisije nikashiba nikakukana,Nikasema, BWANA ni nani?Wala nisiwe maskini sana nikaiba,Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.
10. Usimchongee mtumwa kwa bwana wake;Asije akakulaani, ukaonekana una hatia.
11. Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao;Wala hawambariki mama yao.
12. Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe;Ambao hawakuoshwa uchafu wao.
13. Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini!Na kope zao zimeinuka sana.
14. Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga;Na vigego vyao ni kama visu.Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu.
15. Mruba anao binti wawili,Waliao, Nipe! Nipe!Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe,Naam, vinne visivyosema, Basi!
16. Kuzimu; na tumbo lisilozaa;Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!