Mit. 11:11-22 Swahili Union Version (SUV)

11. Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki;Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.

12. Asiye na akili humdharau mwenziwe;Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.

13. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri;Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.

14. Pasipo mashauri taifa huanguka;Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.

15. Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia;Achukiaye mambo ya dhamana yu salama.

16. Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;Na watu wakali hushika mali siku zote.

17. Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake;Aliye mkali hujisumbua mwili wake.

18. Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu;Apandaye haki ana thawabu ya hakika.

19. Haki huelekea uzima;Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.

20. Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa BWANA;Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.

21. Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu;Bali wazao wa wenye haki wataokoka.

22. Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe,Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili.

Mit. 11