1. Na kwa ajili ya hayo yote, nikatia moyo wangu katika kuyatafuta-tafuta haya; ya kuwa wenye haki, na wenye hekima, pamoja na matendo yao yote, wamo mkononi mwa Mungu; kwamba ni pendo au kwamba ni chuki, mwanadamu hajui; mambo yote yawapita.
2. Mambo yote yawatukia wote sawasawa; kuna tukio moja kwake mwenye haki na kwake asiye haki; kwa mtu mwema na kwa mtu mwovu; kwa mtu aliye safi na kwa mtu asiye safi; kwake yeye atoaye kafara na kwake asiyetoa kafara; kama alivyo huyo mwema ndivyo alivyo mwenye dhambi; yeye aapaye na yeye aogopaye kiapo.
3. Baa hilo ni katika mambo yote yanayofanyika chini ya jua, ya kuwa wote wanalo tukio moja; naam, zaidi ya hayo, mioyo ya wanadamu imejaa maovu, na wazimu umo mioyoni mwao wakati walipo hai, na baadaye huenda kwa wafu.
4. Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai; (maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa);
5. kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa.