1. Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.
2. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini?
3. Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao.
4. Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;
5. nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;
6. nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga.
7. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng’ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu;
8. tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.
9. Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.
10. Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.
11. Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua.
12. Nikageuka ili kuipambanua hekima, na wazimu na upumbavu. Kwa maana mtu amfuataye mfalme afanye nini? Lilo hilo tu lililokwisha kufanywa.
13. Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza;
14. macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa.
15. Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
16. Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu!