1. Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako,Kabla hazijaja siku zilizo mbaya,Wala haijakaribia miaka utakaposema,Mimi sina furaha katika hiyo.
2. Kabla jua, na nuru, na mwezi,Na nyota, havijatiwa giza;Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
3. Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema;Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha;Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba;Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza;
4. Na milango kufungwa katika njia kuu;Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo;Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege;Nao binti za kuimba watapunguzwa;
5. Naam, wataogopa kilichoinukaNa vitisho vitakuwapo njiani;Na mlozi utachanua maua;Na panzi atakuwa ni mzigo mzito;Na pilipili hoho itapasuka;Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele,Nao waombolezao wazunguka njiani.
6. Kabla haijakatika kamba ya fedha;Au kuvunjwa bakuli la dhahabu;Au mtungi kuvunjika kisimani;Au gurudumu kuvunjika birikani;
7. Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa,Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.
8. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!
9. Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.
10. Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli.
11. Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja.
12. Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.
13. Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa;Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.