Mhu. 10:7-18 Swahili Union Version (SUV)

7. Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.

8. Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake;Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma.

9. Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo;Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo.

10. Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi;Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa.

11. Nyoka akiuma asijatumbuizwa,Basi hakuna faida ya mtumbuizi.

12. Maneno ya kinywa chake mwenye hekima yana neema;Bali midomo ya mpumbavu itammeza nafsi yake.

13. Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni upuuzi; na mwisho wa usemi wake ni wazimu wenye hatari.

14. Tena, upumbavu huongeza maneno; lakini mwanadamu hajui yatakayokuwako; nayo yatakayokuwa baada yake, ni nani awezaye kumweleza?

15. Kazi yao wapumbavu huwachosha kila mmoja,Maana hajui hata njia ya kuuendea mji.

16. Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana,Na wakuu wako hula asubuhi!

17. Heri kwako, nchi, mfalme wako akiwa mtoto wa watu,Na wakuu wako hula wakati ufaao, Ili makusudi wapate nguvu, wala si kwa ajili ya ulevi.

18. Kwa sababu ya uvivu paa hunepa;Na kwa utepetevu wa mikono nyumba huvuja.

Mhu. 10