Mdo 7:44-58 Swahili Union Version (SUV)

44. Ile hema ya ushahidi ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawasawa na mfano ule aliouona;

45. ambayo baba zetu, kwa kupokezana, wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya Mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daudi;

46. aliyepata fadhili mbele za Mungu, naye aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.

47. Lakini Sulemani alimjengea nyumba.

48. Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii,

49. Mbingu ni kiti changu cha enzi,Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu;Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana,

50. Au ni mahali gani nitakapostarehe?Si mkono wangu uliofanya haya yote?

51. Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.

52. Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua;

53. ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.

54. Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.

55. Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.

56. Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.

57. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,

58. wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.

Mdo 7