13. Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.
14. Na wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu.
15. Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao,
16. wakisema, Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana.
17. Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili.
18. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.
19. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe;
20. maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.
21. Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka;
22. maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini.
23. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee.
24. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;
25. nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako,Mbona mataifa wamefanya ghasia,Na makabila wametafakari ubatili?
26. Wafalme wa dunia wamejipanga,Na wakuu wamefanya shauri pamojaJuu ya Bwana na juu ya Kristo wake.
27. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta,
28. ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee.
29. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote,
30. ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.