Mdo 24:13-22 Swahili Union Version (SUV)

13. Wala hawawezi kuyahakikisha mambo haya wanayonishitaki sasa.

14. Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii.

15. Nina tumaini kwa Mungu, ambalo hata hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia.

16. Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote.

17. Baada ya miaka mingi nalifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo.

18. Wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, hali nimetakaswa, wala sikuwa na mkutano wala ghasia; lakini walikuwako baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia,

19. ambao imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki, kama wana neno lo lote juu yangu.

20. Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza,

21. isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, na kusema, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo.

22. Basi Feliki aliwaahirisha, kwa sababu alijua habari za Njia ile kwa usahihi zaidi, akasema, Lisia jemadari atakapotelemka nitakata maneno yenu.

Mdo 24