Mdo 16:18-26 Swahili Union Version (SUV)

18. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.

19. Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;

20. wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;

21. tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.

22. Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.

23. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.

24. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale.

25. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

26. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.

Mdo 16