Mdo 13:38-52 Swahili Union Version (SUV)

38. Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi;

39. na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa.

40. Angalieni, basi, isiwajilie habari ile iliyonenwa katika manabii.

41. Tazameni, enyi mnaodharau, kastaajabuni, mkatoweke; kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu, kazi ambayo msingeisadiki kabisa, ijapo mtu akiwasimulia sana.

42. Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili.

43. Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu.

44. Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.

45. Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana.

46. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.

47. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana,Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa,Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.

48. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

49. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.

50. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao.

51. Nao wakawakung’utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio.

52. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.

Mdo 13