1. Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi.
2. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema BWANA wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni.
3. Angalieni, nitaikemea mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam, mavi ya sadaka zenu; nanyi mtaondolewa pamoja nayo
4. Nanyi mtajua ya kuwa mimi nimewapelekeeni amri hii, ili agano langu liwe na Lawi, asema BWANA wa majeshi.
5. Agano langu naye lilikuwa agano la uhai na amani; nami nikampa ili aogope, naye akaniogopa, akalicha jina langu.
6. Sheria ya kweli ilikuwa kinywani mwake, wala udhalimu haukuonekana midomoni mwake; alikwenda pamoja nami katika amani na unyofu, na kuwageuza wengi hata wakaacha uovu.