Lk. 9:35-46 Swahili Union Version (SUV)

35. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.

36. Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona.

37. Ikawa siku ya pili yake, waliposhuka mlimani, mkutano mkubwa ulikutana naye.

38. Na tazama, mtu mmoja katika mkutano alipaza sauti, akisema, Mwalimu, nakuomba umwangalie mwanangu; kwa kuwa yeye ni mwanangu pekee.

39. Na tazama, pepo humpagaa, naye mara hupiga kelele; tena humtia kifafa, huku anatokwa na povu, wala hamwachi ila kwa shida, akimchubua-chubua.

40. Nikawasihi wanafunzi wako wamtoe, wasiweze.

41. Yesu akajibu akasema, Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwachukulia hata lini? Mlete mwanao hapa.

42. Alipokuwa katika kumwendea, pepo akambwaga chini, akamtia kifafa. Yesu akamkemea pepo mchafu, akamponya mtoto, akamrudishia babaye.

43. Wote wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu.Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi wake,

44. Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu.

45. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.

46. Wakaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao.

Lk. 9