32. Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye.
33. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo.
34. Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo.
35. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.
36. Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona.
37. Ikawa siku ya pili yake, waliposhuka mlimani, mkutano mkubwa ulikutana naye.
38. Na tazama, mtu mmoja katika mkutano alipaza sauti, akisema, Mwalimu, nakuomba umwangalie mwanangu; kwa kuwa yeye ni mwanangu pekee.
39. Na tazama, pepo humpagaa, naye mara hupiga kelele; tena humtia kifafa, huku anatokwa na povu, wala hamwachi ila kwa shida, akimchubua-chubua.
40. Nikawasihi wanafunzi wako wamtoe, wasiweze.
41. Yesu akajibu akasema, Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwachukulia hata lini? Mlete mwanao hapa.
42. Alipokuwa katika kumwendea, pepo akambwaga chini, akamtia kifafa. Yesu akamkemea pepo mchafu, akamponya mtoto, akamrudishia babaye.
43. Wote wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu.Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi wake,
44. Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu.
45. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.
46. Wakaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao.
47. Naye Yesu alipotambua mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye,
48. akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa.
49. Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi.
50. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.
51. Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;