16. Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake.
17. Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi.
18. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.
19. Wakamwendea mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano.
20. Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe.
21. Akawajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
22. Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga.
23. Nao walipokuwa wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari.
24. Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia. Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari.
25. Akawaambia, Imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?
26. Wakafika pwani ya nchi ya Wagerasi, inayoelekea Galilaya.
27. Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini.
28. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese.
29. Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo.
30. Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia.
31. Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni.
32. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa.
33. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji.
34. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani.