1. Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene,
2. wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria, jangwani.
3. Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi,
4. kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya;Sauti ya mtu aliaye nyikani,Itengenezeni njia ya Bwana,Yanyosheni mapito yake.
5. Kila bonde litajazwa,Na kila mlima na kilima kitashushwa;Palipopotoka patakuwa pamenyoka,Na palipoparuza patalainishwa;
6. Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.
7. Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?
8. Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto.
9. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
10. Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi?