11. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
12. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.
13. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
14. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
15. Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea.
16. Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao.
17. Amin, nawaambia, Mtu ye yote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe.
18. Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele?
19. Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu.
20. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako.
21. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu.
22. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate.
23. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi.
24. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!
25. Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.