Lk. 12:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo.

6. Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu.

7. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

8. Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu;

9. na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.

10. Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11. Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema;

12. kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema.

13. Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.

14. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?

15. Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.

16. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;

17. akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.

18. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.

Lk. 12