Lk. 12:30-42 Swahili Union Version (SUV)

30. kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo.

31. Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa.

32. Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.

33. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.

34. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu.

35. Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;

36. nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.

37. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia.

38. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.

39. Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa.

40. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.

41. Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?

42. Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake?

Lk. 12