4. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu].
5. Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,
6. kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;
7. na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?
8. Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.
9. Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
10. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12. Au akimwomba yai, atampa nge?
13. Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?
14. Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu.
15. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.
16. Wengine walimjaribu, wakimtaka ishara itokayo mbinguni.
17. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka.