34. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza.
35. Angalia basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.
36. Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga wake.
37. Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani.
38. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula.
39. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu.
40. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia?
41. Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.