Law. 9:13-24 Swahili Union Version (SUV)

13. Nao wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, na kichwa; naye akaviteketeza juu ya madhabahu.

14. Kisha akaosha matumbo, na miguu na kuiteketeza juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa madhabahuni.

15. Kisha akaisongeza dhabihu ya watu, akamtwaa mbuzi wa sadaka ya dhambi aliyekuwa kwa hao watu, na kumchinja, na kumtoa kwa ajili ya dhambi kama yule wa kwanza.

16. Kisha akaisongeza sadaka ya kuteketezwa, na kuitoa sawasawa na sheria.

17. Kisha akaisongeza sadaka ya unga, na kutwaa konzi humo, na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.

18. Huyo ng’ombe mume naye akamchinja, na huyo kondoo mume pia, dhabihu ya sadaka za amani, zilizokuwa kwa ajili ya watu; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote,

19. na mafuta ya ng’ombe; na ya kondoo, mkia wake wa mafuta, na hayo yafunikayo matumbo, na figo zake, na kitambi cha ini;

20. nao wakayaweka hayo mafuta juu ya vidari, naye akayateketeza mafuta juu ya madhabahu;

21. na vile vidari, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume, Haruni akavitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele ya BWANA; kama Musa alivyoagiza.

22. Kisha Haruni akainua mikono yake na kuielekeza kwa hao watu, akawabariki; kisha akashuka akisha isongeza sadaka ya dhambi, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani.

23. Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo utukufu wa BWANA ukawatokea watu wote.

24. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.

Law. 9