23. Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume.
24. Kisha akawaleta wana wa Haruni, na Musa akaitia hiyo damu katika ncha za masikio ya kuume, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vya gumba vya maguu yao ya kuume; kisha Musa akainyunyiza hiyo damu katika madhabahu pande zote.
25. Kisha akayatwaa hayo mafuta, na mkia wenye mafuta, na mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo, na kitambi cha ini, na figo mbili, na mafuta yake, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume;
26. kisha katika kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichokuwa pale mbele za BWANA, akatwaa mkate mmoja usiochachwa, na mkate mmoja ulioandaliwa na mafuta na kaki moja nyembamba, akaiweka juu ya mafuta, na juu ya huo mguu wa nyuma wa upande wa kuume;
27. kisha akaweka vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe, na kuvitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA.
28. Kisha Musa akavitwaa tena mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa vilikuwa vya kuwaweka wakfu, ni harufu nzuri; ilikuwa dhabihu iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto.
29. Kisha Musa akakitwaa kile kidari, akakitikisa huku na huku, kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; ni sehemu ya Musa katika huyo kondoo mume wa kuwaweka wakfu; kama BWANA alivyomwagiza Musa.
30. Kisha Musa akatwaa baadhi ya mafuta ya kutia, na ya damu iliyokuwa pale juu ya madhabahu, na kumnyunyizia Haruni, katika mavazi yake, na wanawe, katika mavazi yao, pamoja naye; akamtakasa Haruni, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.
31. Kisha Musa akawaambia huyo Haruni na wanawe, Tokoseni hiyo nyama mlangoni pa hema ya kukutania; mkaile pale pale, na hiyo mikate iliyo katika kile kikapu cha kuwaweka wakfu, kama nilivyoagizwa kusema, Haruni na wanawe wataila.
32. Nacho kitakachosalia katika hiyo nyama na mikate mtakichoma moto.
33. Wala msitoke nje mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba, hata siku za kuwekwa wakfu kwenu zitakapotimia; kwa kuwa atawaweka muda wa siku saba.
34. Vile vile kama vilivyotendeka siku ya leo, ni vivyo BWANA alivyoagiza kufanywa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.