1. BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2. Mtwae Haruni, na wanawe pamoja naye, na yale mavazi, na mafuta ya kutia, na ng’ombe mume wa sadaka ya dhambi, na kondoo waume wawili, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu;
3. kisha ukutanishe mkutano wote hapo mlangoni pa hema ya kukutania.
4. Basi Musa akafanya kama alivyoambiwa na BWANA; na huo mkutano ulikutanishwa mlangoni pa hema ya kukutania.
5. Musa akawaambia mkutano, Neno aliloliagiza BWANA kwamba lifanywe, ni hili.
6. Basi Musa akawaleta Haruni na wanawe, akawaosha kwa maji.
7. Kisha akamvika Haruni ile kanzu, na kumfunga mshipi, na kumvika joho, na kumvika naivera, na kumfunga huo mshipi wa kazi ya mstadi wa naivera na kumfunga naivera kwa huo mshipi.
8. Kisha akamtia kile kifuko cha kifuani; akatia hizo Urimu na Thumimu katika hicho kifuko cha kifuani.
9. Akamvika na kile kilemba kichwani mwake; na juu ya kilemba, upande wa mbele, akakitia kile kipande cha dhahabu, hiyo taji takatifu; kama BWANA alivyomwagiza Musa.
10. Kisha Musa akatwaa hayo mafuta matakatifu ya kutia, akatia mafuta maskani, na vyote vilivyokuwamo, na kuvitakasa.
11. Kisha akanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kuitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake, ili kuvitakasa.
12. Kisha akamimina mafuta hayo ya kutia kichwani mwake Haruni, na kumtia mafuta, ili amtakase.
13. Kisha Musa akawaleta wana wa Haruni, na kuwavika kanzu, na kuwafunga mishipi, na kuwavika vilemba; kama BWANA alivyomwagiza Musa.
14. Kisha akamleta yule ng’ombe mume wa sadaka ya dhambi; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao katika kichwa cha huyo ng’ombe wa sadaka ya dhambi.
15. Kisha akamchinja; na Musa akaitwaa damu yake, akaitia katika pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake, akaitakasa madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu, na kuitakasa, ili afanye upatanisho kwa ajili yake.
16. Kisha akayatwaa mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo yake, na kitambi kilichokuwa katika ini, na figo zake mbili, na mafuta yake, na Musa akayateketeza juu ya madhabahu.