21. Na huyo mume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa BWANA, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo mume kwa hiyo sadaka ya hatia.
22. Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia mbele za BWANA, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya.
23. Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni kutotahiriwa; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa.
24. Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa BWANA shukrani.
25. Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa maongeo yake; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
26. Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.
27. Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu.
28. Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA.
29. Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu.
30. Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi BWANA.
31. Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
32. Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi BWANA.
33. Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu.
34. Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
35. Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo.
36. Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri.
37. Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi BWANA.