1. BWANA akanena na Musa, akamwambia,
2. Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu.
3. Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
4. Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
5. Nanyi hapo mtakapomchinjia BWANA sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa.
6. Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto.
7. Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa;
8. lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha BWANA; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.