3. Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya.
4. Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya marago.
5. Basi wakaja karibu, na kuwachukua, hali wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya marago; kama Musa alivyosema.
6. Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe Eleazari na Ithamari, Msiache wazi nywele za vichwani mwenu, wala msiyararue mavao yenu; ili kwamba msife, tena asiukasirikie mkutano wote; lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, na waomboleze kwa ajili ya hicho kichomo alichowasha BWANA.
7. Wala hamtatoka nje mlangoni mwa hema ya kukutania, msije mkafa; kwa sababu mafuta ya kutiwa ya BWANA ya juu yenu. Nao wakafanya kama hilo neno la Musa.
8. Kisha BWANA akanena na Haruni, na kumwambia,
9. Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu;
10. kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi;
11. tena mpate kuwafundisha wana wa Israeli amri hizi zote ambazo BWANA amewaambia kwa mkono wa Musa.