17. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao?
18. Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa.
19. Basi sasa tuma wahimize waingie ndani wanyama wako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa.
20. Yeye aliyelicha neno la BWANA miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani;
21. na yeye asiyelitia moyoni neno la BWANA akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani.
22. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri.
23. Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na BWANA akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri.
24. Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa.
25. Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba.
26. Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe.
27. Farao akatuma watu, na kuwaita Musa na Haruni, na kuwaambia, Mimi nimekosa wakati huu; BWANA ni mwenye haki, na mimi na watu wangu tu waovu.
28. Mwombeni BWANA; kwa kuwa zimekuwa za kutosha ngurumo hizo kuu na hii mvua ya mawe; nami nitawapa ninyi ruhusa mwende zenu, msikae zaidi.
29. Musa akamwambia, Mara nitakapotoka mjini nitamwinulia BWANA mikono yangu; na hizo ngurumo zitakoma, wala haitanyesha mvua ya mawe tena; ili upate kujua ya kuwa dunia hii ni ya BWANA.
30. Lakini, wewe na watumishi wako, najua ya kuwa ninyi hamtamcha BWANA Mungu bado.
31. Kitani na shayiri zilipigwa; maana shayiri zilikuwa na masuke na kitani zilikuwa katika kutoa maua.
32. Lakini ngano na kusemethu hazikupigwa; maana, zilikuwa hazijakua bado.
33. Musa akatoka mjini, kutoka kwa Farao, akamwinulia BWANA mikono yake; na zile ngurumo na ile mvua ya mawe zikakoma, wala mvua haikunyesha juu ya nchi.
34. Farao alipoona ya kwamba mvua na mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akazidi kufanya dhambi, na kuufanya moyo wake mzito, yeye na watumishi wake.
35. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu naye hakuwapa wana wa Israeli ruhusa waende zao; kama BWANA alivyonena kwa kinywa cha Musa.