3. Nawe utatia ndani yake sanduku la ushuhuda, nawe utalisitiri hilo sanduku kwa pazia.
4. Nawe utaleta meza na kuitia ndani, na kuviweka sawasawa vile vitu juu yake; kisha utakileta ndani kile kinara cha taa, na kuziwasha taa zake.
5. Kisha utaisimamisha madhabahu ya dhahabu kwa kufukizia uvumba mbele ya sanduku la ushuhuda, na kulitia pazia mlangoni mwa hiyo maskani.
6. Kisha utaweka madhabahu ya kuteketeza sadaka mbele ya mlango wa maskani ya hema ya kukutania.
7. Kisha utaliweka birika kati ya hema ya kukutania na hiyo madhabahu, nawe utatia maji ndani yake.
8. Kisha utausimamisha ukuta wa ua kuuzunguka pande zote, na kuitundika sitara ya lango la ua.
9. Kisha utayatwaa mafuta ya kutiwa, na kuitia mafuta hiyo maskani, na kila kitu kilicho ndani yake, na kuiweka iwe takatifu, na vyombo vyake vyote; nayo itakuwa takatifu.
10. Kisha utaitia mafuta madhabahu ya kuteketeza sadaka, na vyombo vyake vyote; na kuiweka takatifu madhabahu; na hiyo madhabahu itakuwa takatifu sana.
11. Kisha utalitia mafuta birika na tako lake, na kuliweka liwe takatifu.
12. Kisha utamleta Haruni na wanawe hapo mlangoni pa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji.
13. Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani.
14. Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao;
15. nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote.