1. BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2. Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza utaisimamisha hiyo maskani ya hema ya kukutania.
3. Nawe utatia ndani yake sanduku la ushuhuda, nawe utalisitiri hilo sanduku kwa pazia.
4. Nawe utaleta meza na kuitia ndani, na kuviweka sawasawa vile vitu juu yake; kisha utakileta ndani kile kinara cha taa, na kuziwasha taa zake.
5. Kisha utaisimamisha madhabahu ya dhahabu kwa kufukizia uvumba mbele ya sanduku la ushuhuda, na kulitia pazia mlangoni mwa hiyo maskani.
6. Kisha utaweka madhabahu ya kuteketeza sadaka mbele ya mlango wa maskani ya hema ya kukutania.
7. Kisha utaliweka birika kati ya hema ya kukutania na hiyo madhabahu, nawe utatia maji ndani yake.
8. Kisha utausimamisha ukuta wa ua kuuzunguka pande zote, na kuitundika sitara ya lango la ua.