Kut. 4:12-21 Swahili Union Version (SUV)

12. Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena.

13. Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma.

14. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake.

15. Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya.

16. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake.

17. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.

18. Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani.

19. BWANA akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, karudi Misri; kwa kuwa wale watu wote waliokutaka uhai wako wamekwisha kufa.

20. Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.

21. BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao.

Kut. 4