1. Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia BWANA ni haya, kwamba myafanye.
2. Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa BWANA; mtu awaye yote atakayefanya kazi yo yote katika siku hiyo atauawa.
3. Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato.
4. Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru BWANA, akisema,
5. Katwaeni kati yenu matoleo kwa BWANA; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba;