17. Usijifanyizie miungu ya kuyeyusha.
18. Hiyo sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu utaitunza. Utakula mikate isiyotiwa chachu muda wa siku saba, kama nilivyokuagiza, kwa majira yaliyoaganwa katika mwezi wa Abibu; kwa kuwa ulitoka Misri katika mwezi huo wa Abibu.
19. Kila kifunguacho mimba ni changu mimi; na wanyama wako wote walio waume, wazaliwa wa kwanza wa ng’ombe na wa kondoo.
20. Na mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; tena kwamba hutaki kumkomboa, ndipo utamvunja shingo. Wazaliwa wa kwanza wote wa wanao utawakomboa. Wala hapana atakayehudhuria mbele zangu mikono mitupu.
21. Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika.
22. Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka.
23. Mara tatu kila mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli.
24. Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu ye yote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za BWANA Mungu wako mara tatu kila mwaka.
25. Usisongeze damu ya sadaka yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu; wala hiyo sadaka ya sikukuu ya pasaka haitasazwa hata asubuhi.
26. Vitu vya kwanza vya malimbuko ya nchi yako utavileta na kuvitia ndani ya nyumba ya BWANA Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
27. BWANA akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya.
28. Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.
29. Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling’aa kwa sababu amesema naye.
30. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia.
31. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao.