Kut. 30:22-36 Swahili Union Version (SUV)

22. Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

23. Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na kane shekeli mia mbili na hamsini,

24. na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano;

25. nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa.

26. Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda,

27. na hiyo meza, na vyombo vyake vyote, na kinara cha taa, na vyombo vyake, na madhabahu ya kufukizia uvumba,

28. na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na tako lake.

29. Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu.

30. Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, na kuwatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.

31. Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote.

32. Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu.

33. Mtu awaye yote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu awaye yote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.

34. BWANA akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja;

35. nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenazaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu;

36. nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana.

Kut. 30